DK. MWINYI: SERIKALI INAFANYA JUHUDI KUZIBA MIANYA YA WIZI WA MALI ZA SERIKALI

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa juhudi za makusudi zimechukuliwa na Serikali anayoiongoza katika kuziba mianya ya wizi wa fedha za serikali.

 


Alisema kuwa hatua hiyo ameichukua kwa sababu anataka fedha za Serikali ziingie katika mfuko wa Serikali ili ziweze kuwafaidisha wananchi walio wengi badala ya wale wachache.

 

Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akitoa salamu zake kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wote mara baada ya Sala ya Ijumaa huko Masjid Mahfoudh uliopo Mazizini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

 

Alisema kuwa kuna kundi ambalo hatua hizo zilizochukuliwa na Serikali zimewaathiri lakini hata hivyo ameahidi kuendelea kuchukua hatua kwani lengo lake ni kuhakikisha fedha zinazotakiwa kuingia Serikali zinaingia ili ziweze kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo maji, elimu, miundombinu ya barabara, umeme na miradi mengineyo.

 

Hivyo, Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba ni lazima mapato ya Serikali yasimamiwe ipasavyo ili yaweze kutumika kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi walio wengi.

 

Akieleza kuhusu suala zima la kuimarisha amani, Alhaji Dk. Mwinyi alisema kwamba kila mmoja anapaswa kuhubiri suala la amani, kwani amani ni msingi wa mambo yote yakiwemo ya kidini, kijamii na kiuchumi huku akisisitiza kwamba nchi imo katika amani.

 

Alieleza kwamba mara nyingi amani hapa nchini hutetereka wakati wa uchanguzi, hivyo ni vyema kumuomba Mwenyezi Mungu hata ukifika wakati huo wa uchaguzi amani iendelee kudumu ili wananchi waendelee kutekeleza majukumu yao na kuishi kwa salama.

 

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba suala la kupambana na vitendo viovu katika jamii ikiwemo udhalilishaji wa wanawake na watoto pamoja na matumizi ya dawa za kulevya yanapaswa kupigwa vita kwa mashirikiano ya pamoja ili jamii iendelee kukaa katika mafundisho ya dini.

 

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa kutokea kwa janga la ugonjwa wa COVID 19 ni mtihani wa Mwenyezi Mungu kwani halikuathiri afya za watu pekee  bali kwa kiwango kikubwa limeathiri uchumi wa mataifa.

 

Alisema kuwa wakati janga hilo liliposhamiri nchi nyingi duniani zilifunga mipaka yao na kupelekea uzalishaji kushuka na kupungua ambapo hivi sasa bidhaa hizo zimepanda bei sambamba na gharaza za usafirishaji nazo kuongezeka, hivyo aliwataka wananchi kuwa wavumilivu kwani hali hiyo itamaliza.

 

Alisema kuwa ugonjwa huo utapita na hali ya kawaida itarudi na Serikali itahakikisha kwa wale ambao hawatotaka kushusha bei za bidhaa sababu hiyo haitakuwepo hivyo, hatua stahiki itachukuliwa ili kuweza kurudi katika hali ya kawaida.

 

Aliwahakikishia wananchi kwamba wepesi utakuja na kuwaomba waendelee kumuomba Mwenyezi Mungu ili ugonjwa wa COVID 19 uondoke kabisa.

 

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi alipokea ombi la uongozi wa msikiti huo la kusaidia ujenzi wa jengo lao la Chuo cha msikiti liliopo pembezoni mwa msikiti huo.

 

Mapema akisoma hotuba ya Sala ya Ijumaa, Khatibu wa msikiti huo Sheikh Ali Abdulrahman alisisisitiza haja kwa waumini wa dini ya Kiislamu kuendelea kutenda mambo mema pamoja na kuwaenzi viongozi huku akiwakumbusha waumini juu ya kupiga vita udhalilishaji wa kijisia kwa wananawake na watoto.