KESI 96 ZA UKATILI NA UDHALILISHAJI ZARIPOTIWA NDANI YA MWEZI AGOSTI

 Jumla ya matukio 96 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa mwezi wa Agosti ,2021 ambapo wengi wao walikuwa ni  watoto asilimia 90.6 na wanawake ni asilimia9.4.

Akiwasilisha  takwimu za Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia kwa wanawake na  Watoto Mtakwimu Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali katika Kitengo cha Makosa ya Jinai,Madai  na Jinsia Ramla Hassan  Pandu wakati alipokuwa akizungumza na waandishi  wa  habari huko  katika ukumbi wa Mtakwimu  Mkuu wa Serikali uliopo Mazizini.

Amesema Mlinganisho wa  idadi  ya  matukio kwa Mwezi imepungua  kwa  asilimia  11.1 kutoka  matukio  108  kwa  mwezi wa  Julai,2021 hadi 96 mwezi wa Agosti 2021.

Aidha amesema Wilaya ya Magharibi “A” imeripotiwa kuwa na matukio  mengi  ukilinganisha  na  Wilaya  nyengine  ambapo matukio  25 ikifuatiwa  na Wilaya  ya Magharibi “B” Matukio 20  ambapo  Wilaya ya  Kaskazini “A” Micheweni na Mkoani zimeripotiwa kuwa na idadi  ndogo zaidi  ya  matukio kuliko  wilaya zote matukio mawili 2 kwa kila wilaya.

Muwasilishaji huyo amesema  matukio 90 yapo chini ya upelelezi wa Polisi na matukio 6 yapo katika hatua nyengine ambapo matukio 4 manne  yapo Mahakamani na matukio mawili 2 yapo Ofisi ya Mashitaka.

Kwa  upande wake Mrakibu Msaidizi  wa Polisi  Mkuu wa Kitengo cha Takwimu Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Ramadhani Himidi amesema Jeshi la Polisi linatoa wito kwa jamii kuendelea  kushirikiana katika kutokomeza vitendo vya udhalilishaji ili viweze kumalizika.

Nae Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii Wanawake na Watoto kutoka Kitengo cha Watoto Mohamed Jabir amesema ili tatizo hilo lisiendelee taaluma  itolewe kwa wazazi wawe karibu na watoto na kuwaelimisha ili waweze kujinusuru pale  watapofikwa na kadhia hiyo waweze kuepukana nayo.