MKURUGENZI MKUU WA NEMC AFANYA ZIARA KWENYE ENEO OEVU LINALOATHIRIWA NA SHUGHULI ZA KIBINADAMU WILAYANI KIBAHA

 

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka amesema Baraza  limebaini kuwa kuna maendeleo yamefanyika katika mji wa Mlandizi ikiwa ni pamoja na Viwanda na Ofisi za Halmashauri zilizojengwa bila kufanyika tafiti za Kimazingira.

 

Ameyasema hayo alipotembelea Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, ambapo amesema Serikali ilitoa eneo hilo kwa Halmashauri ya Kibaha kwa ajili ya kuendeleza mji.

 

‘‘Maendeleo ya Halmashauri na Viwanda katika mji huu zimejengwa bila kufanyika utafiti wowote wa Kimazingira. Lakini athari zake ni kwamba hili eneo ni Oevu, Maeneo oevu katika Sheria ya Mazingira inasema ni maeneo yanayotakiwa kutengwa na kulindwa kwa ajili ya kuhifadhi ikolojia ya mahali hapo. Ikolojia ya mahali hapa ni Bonde pana  hivyo  wakati wa mvua na mafuriko linahifadhi maji na kuchuja sumu zilizo kwenye maji kwa ajili ya kutiririsha baharini. Mito wakati wa kiangazi hupokea maji yaliyohifadhiwa mabondeni, hivyo tukiharibu mazingira kwa kujenga viwanda, makazi pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu tutasabisha ukosefu mkubwa wa maji wakati wa kiangazi hasa katika eneo hili la Pwani na Dar es Salaam linalotegemea mto Ruvu’’ Dkt. Samuel Gwamaka amesema

 


Aidha alisema kuwa, mabonde ni  matenki ya asili na kazi yake ni kuhifadhi na kuchuja maji  yanayoingia ardhini ili wakati wa kiangazi viumbe hai waendelee kupata maji hivyo yakiharibiwa mazingira madhara yake ni makubwa kwa kizazi kijacho, hivyo ni lazima kuyatunza  kwa ajli ya kulinda uhai wa viumbe  vyote pamoja na mimea.