Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema
katika bajeti ya mwaka 2021/2022 Serikali itajenga bwawa la kunyweshea Mifugo
lenye thamani ya Shilingi Milioni 480 katika Kijiji cha Kimambi, Wilayani
Liwale, Mkoani Lindi.
Ulega aliyasema hayo Septemba 20, 2021 alipofanya ziara
katika Wilaya ya Liwale, Mkoani Lindi kwa lengo la kusikiliza kero za Wafugaji
na Wakulima ili kuzitatua.
Alisema ujenzi wa bwawa hilo utasaidia kutatua changamoto ya
maji ambayo inawakabili wafugaji wa maeneo hayo na utasaidia pia kutatua
migogoro baina yao na wakulima Wilayani humo.
"Rais Samia Suluhu Hassan anakwenda kuwajengea bwawa
lenye thamani ya Shilingi Milioni 480 hapa Kimambi, ujenzi wa bwawa hilo
utasaidia kuwaondosha katika migogoro," alisema Ulega
Naibu Waziri Ulega alisisitiza kuwa pesa hizo zipelekwe kufanya kazi iliyopangiwa
ya ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo huku akiwataka viongozi wa Wilaya hiyo
kuhakikisha pesa hizo zinatumika vizuri.
Aidha, alisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amewapa pia
Majosho mawili katika Kijiji cha Kimambi na Kijiji cha Luwele.
"Sasa kwa sababu huku mifugo imekuwa mingi sana, Mimi nakuongezeeni Josho
lingine hapa ili mifugo mingi iweze kuogeshwa ," aliongeza Ulega
Naye, Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka alitumia nafasi hiyo
kumshukuru Rais wa Awamu ya Sita, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea pesa
hizo huku akisema kuwa bwawa hilo likikamilika hawatarajii tena kuona migogoro
katika Vijiji vilivyotengwa kwa ajili ya Wafugaji Wilayani humo.