Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa
Rais, Dkt. Andrew Komba amesema nyenzo kubwa ya kupunguza matumizi ya Zebaki
kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu ni kutoa elimu kwa kundi hilo.
Dkt. Komba amesema hayo wakati akifungua warsha ya kukuza uelewa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa
Mpango kazi wa kupunguza matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu
(2020 -2025), iliyofanyika jijini Dodoma.
Alisema
Tanzania ilitekeleza mradi wa kuandaa Mpango kazi wa Taifa wa Kupunguza
Matumizi ya Zebaki ambao ni wa miaka mitano (2020 – 2025) kwa lengo la kupunguza
na pale inapowezekana kuondosha matumizi ya kemikali hiyo katika shughuli za
wachimbaji wadogo wa dhahabu ili kulinda afya ya binadamu na mazingira.
Aidha,
Dkt. Komba alisema pamoja na kuwa na lengo kuu la kupunguza matumizi ya Zebaki
vilevile unalenga kuendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia mbadala ili
kupunguza changamoto za afya ya binadamu na mazingira kwa ujumla.
“Uchimbaji
huu mdogo wa dhahabu nchini hutumia kemikali ya Zebaki katika kuchenjua
dhahabu. Pamoja na faida kubwa inayopatikana kutokana na sekta hii, shughuli
hizi zimekuwa na changamoto kubwa katika afya ya binadamu na mazingira ikiwa ni
pamoja na umwagaji maji yenye sumu kwenye mazingira, uchafuzi wa hewa
unaotokana na uchomaji holela wa dhahabu, uchenjuaji wa dhahabu usiotumia vifaa
kinga, ukataji wa miti kwa ajili ya kupata magogo ya kujengea mashimo,” alisema
Dkt. Komba.
Mkurugenzi
huyo alisema tafiti mbalimbali zimeendelea kufanyika na kubainisha kuwa Zebaki
ni chanzo kimojawapo cha uchafuzi wa mazingira duniani ambapo huchangia
takriban asilimia 38 ya uchafuzi wa mazingira na hali inaambatana na athari
katika afya ya binadamu.
Aidha,
kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Zebaki inatajwa kuwa ni miongoni
mwa vyanzo 10 hatarishi kwa afya ya binadamu hivyo kutokana na hali hiyo,
Jumuiya ya kimataifa ilipitisha Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki mwaka 2013
wenye madhumuni ya kulinda afya ya binadamu dhidi ya madhara ya uchafuzi wa mazingira
unotokana na Zebaki.
Hivyo,
Mpango Kazi huo umeainisha pamoja na mambo mengine Hali ya Sekta ya Wachimbaji Wadogo nchini ilivyo; Malengo
na Shabaha Muhimu ya Mpango–Kazi;
Mikakati ya Utekelezaji ikihusisha Gharama na Utaratibu wa Utekelezaji;
na Uratibu wa Tathmini na Ufuatiliaji.