Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali
Mwinyi ameeleza
kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa yakiwemo Mabaraza ya Miji na Manispaa za Zanzibar.
Rais ameyasema hayo alipokutana na viongozi
wa Serikali za Mitaa kutoka mikoa yote ya Zanzibar wakiwemo Wakuu wa Mikoa na
Wakuu wa Wilaya zote za Unguja na Pemba, Ikulu Zanzibar.
alieleza kwamba lengo la kikao
hicho ni kuhakikisha mabadiliko chanya yanatokea hasa katika Halmashauri za Unguja
na Pemba sambamba na kuimarisha utendaji wa kazi kwa azma ya kuwahudumia ipasavyo
wananchi.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dk.
Mwinyi alieleza haja kwa kila Halmashauri ihakikishe inatekeleza ipasavyo majukumu
yake ikiwa ni pamoja na kuzisimamia fedha za makusanyo ya mapato na kuwataka
Wakuu wa Mika na Wilaya kusimamia hilo ili fedha hizo ziweze kusaidia shughuli za
maendeleo.
Rais Dk. Mwinyi aliyaeleza majukumu
ya Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na kusimamia suala zima la usafi katika maeneo yote ya
Miji ya Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar ni eneo maarufu la utalii.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza
kwamba makusanyo ya Halmashauri ni lazima yatumike kwa ajili ya maendeleo ya
nchi na wananchi wake.
Rais Dk. Mwinyi alieleza jukumu la
Manispaa zote za Unguja na Pemba katika kuhakikisha miji inakuwa safi huku
akiutaka uongozi wa Tamisemi kuwashajiisha wananchi kufanya usafi katika maeneo
yote wanayoishi yakiwemo maeneo ya biashara.
Alieleza haja kwa wafanyabiashara
wadogo wadogo kupangwa vizuri na
kusisitiza kufanya biashara katika maeneo maalum yaliyopangwa.
Rais Dk. Mwinyi pia, alieleza azma
yake ya kuendelea kuwasaidia na kuwaunga mkono Wajasariamali kwa kutoa kiasi
cha fedha zipatazo Bilioni 70 zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF)
kwa ajili ya kuwasaidia ambapo wenye jukumu la kusimamia fedha hizo ni Serikali
za Mitaa.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Miwnyi
alieleza jukumu la Uongozi wa Mikoa na Wilaya la kusimamia suala zima la ulinzi
na usalama ili kuhakikisha vitendo viovu vinakomeshwa katika jamii.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi
alisisitiza haja kwa Masheha wa Shehia zote za Unguja na Pemba kutekeleza
shughuli zao kwa uadilifu zaidi ili kuweza kuwatumikia wananchi ipasavyo katika
maeneo yao.
Nao viongozi hao wa Serikali za Mitaa
walitoa pongezi zao kwa Rais Dk. Mwinyi kwa maelekezo mazuri aliyowapa pamoja
na kuwatia moyo katika utendaji wao wa kazi na kuahidi kuleta mabadiliko katika
kipindi kifupi kijacho.