Ukuaji wa maendeleo ya Nchi Kiuchumi unachangia changamoto
mbalimbali katika Mazingira kama, mabadiliko ya tabia ya Nchi, kelele na
mitetemo na changamoto nyingine zinazohatarisha Mazingira.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano na Mazingira) Mh.Hamad Hassan
Chande, wakati akifungua Warsha kwa Wamiliki wa Kumbi za Starehe, Bendi za
Muziki , Baa na Wadau wa Muziki. Warsha hiyo imefanyika katika ukumbi wa
Kisenga Millenium Tower jijini Dar es Salaam na imeandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC).
Alisema kwa sababu ya
Changamoto hizo ameona ni vizuri kukutana na wadau hao ili wapatiwe elimu kuhusu kelele
na mitetemo ili kulinda na kuokoa Mazingira na afya ya vizazi vilivyopo na
vijavyo.
“ tumeona kuna umuhimu mkubwa wa kukutana pamoja ili kutoa
elimu kuhusu kelele na mitetemo ili
kulinda Mazingira na afya ya vizazi vyetu vya sasa na vijavyo”. Amesema
Mhe.Chande
Aidha ameongeza kuwa kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na
ongezeko kubwa la kelele na mitetemo katika maeneo yanayozunguka jamii zinazotokana na shughuli
mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
“Tafiti mbalimbali Duniani na hapa nchini zimefanyika
zinaonyesha kwa sasa kelele na mitetemo ni changamoto kubwa inayokuja kuathiri
afya za Wananchi wetu. Mfano, Shirika la Afya Duniani(WHO) limebainisha
keleleni ni kisababishi cha madhara katika Maisha ya binadamu. Aidha, “European
Environmental Agency” katika ripoti yao ya mwaka 2018 imeonyesha kuwa kelele
inachangia vifo vya mapema vya Watoto, Watoto takribani 12000
kila mwaka hufariki katika Bara la Ulaya”.
Alitanabaisha kuwa hapa Nchini pia kuna tafiti zinaendelea
na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wameanza
jitihada hizo katika Kanda mbalimbali, Mfano NEMC Kanda ya Kaskazini wamefanya
tafiti ndogo kuhusu kelele na mitetemo katika Mkoa wa Arusha, tafiti hii
imeonyesha kuwa kelele na mitetemo imekuwa changamoto kubwa katika jamii.
Wananchi wengi wameonyesha kuathirika moja kwa moja na athari za kelele na
mitetemo. Katika tafiti hii, maeneo yaliyo ongoza kwa kusababisha kelele
chafuzi ni maeneo ya starehe kwa 33% na Viwanda 24%.
Amezitaja baadhi ya
athari za kelele na mitetemo kwa jamii zetu ni kama: kuathirika kwa
akili na kusababisha wasiwasi, msongo, hofu, kichefuchefu, maumivu ya kichwa,
ubishi, mabadiliko ya hisia kwenye tendo la ndoa “sexual impotence”, Kuharibika
kwa utendaji wa kazi na matatizo ya kupoteza kumbukumbu na Usumbufu wa usingizi ambapo hali hii
husababisha kuwa na shinikizo la damu, mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida hutokea
(haraka au polepole).
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Muhandisi Samuel Gwamaka,
akiongea katika Warsha hiyo amesema kuwa
kwa kipindi cha hivi karibuni Baraza limepokea taarifa nyingi za
malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali juu ya matukio yanayohusiana na
kelele na mitetemo. Hivyo basi ndiyo maana Baraza limeamua kuandaa warsha hiyo
kwa Wadau hao kuhusiana na kelele na mitetemo.
”Katika kulitafutia ufumbuzi jambo hili kwa kushirikiana na
Wizara mbalimbali, kwa pamoja kama
serikali tumekubaliana kelele na mitetemo ni janga linalokuja kwa kasi katika
jamii yetu. Pamoja na kuwepo Sheria mbalimbali za kisekta, pia tumeandaa Mwongozo
wa udhibiti wa uchafuzi wa Mazingira utokanao na Kelele na Mitetemo ambao
unaonesha muundo wa wadau wa utekelezaji wa udhibiti kelele na mitetemo”.
Alimalizia Dkt Gwamaka.