MAMA ALIYETELEKEZA MTOTO WA MIEZI NANE AKAMWATWA

 


Idara ya Ustawi wa Jamii Zanzibar imemkamata Mama Mzazi wa mtoto aliyetelekeza mwenye umri wa miezi minane  kwa kumuacha nyumbani bila ya kumpa huduma yoyote huko maeneo ya Kianga Wilaya Magharibi “A” Unguja.

Mama huyo anaejulikana kwa jina la Dorice Moses Mazigu mwenye umri wa miaka 27 alikamatwa leo huko Mbuzini  Wilaya ya Magharibi A katika kumbi za starehe  na Idara ya Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na masheha wa shehia ya Kianga  na Mbuzini.

Akizunguza na waandishi wa habari mara baada ya kupatikana mama huyo  huko Welezo Mkurugenzi wa Idara ya Ustawi wa Jamiii na Wazee Abdalla Saleh Omar huko Ofisini kwake, amesema Mama huyo yuko chini ya uangalizi wa vyombo vya sheria kwa ajili ya hatua za kisheria.  

Nae Afisa Ustawi wa Jamii katika kitengo cha Hifadhi ya Mtoto Ramadhan Mohamed Ramadhan amesema hali ya mtoto huyo imedhoofika kutokana na kukosa huduma za mama na uangalizi mazuri.

Ameeleza kuwa mtoto huyo anapatiwa huduma  katika hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja  kwa matibabu ambae anasumbuliwa na vidonda pamoja na tatizo la utapia mlo yuko chini Idara ya Ustawi wa Jamii kwa huduma.

Story na Pili Ali-  Maelezo Zanzibar.