OFISI YA MUFTI MKUU YAIFUNGA MADRASA BAADA YA MWALIMU KUFANYA UDHALILISHAJI KWA WANAFUNZI

 

Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “A”, Suzan Peter Kunambi, amelaani vikali kitendo cha udhalilishaji kilichofanywa na mwalimu wa Madrasa ya Bismilahi iliyoko Mwera Nguzo Mbili, na kuunga mkono hatua iliyochukuliwa na Ofisi ya Mufti kwa kuifungia madrasa hiyo.  

Akizungumza mara baada ya zoezi la kufungwa madrasa hiyo huko Mwera Nguzo Mbili, Mkuu huyo amesema kitendo cha mwalimu kuwafanyia udhalilishaji baadhi ya wanafunzi ni kinyume na maadili ya kazi ya ualimu na ni miongoni mwa tabia mbaya zinazoendelea kupingwa vita nchini.

Alisema wakati wa sasa sio wakati wa kuaminiana, hivyo ipo haja kwa kila mzazi kuwa muangalifu kwa mototo wake na kumlinda, ili kumuepusha na vitendo viovu.

 “Wazazi lazima tuwe waangalifu huu si wakati wa kumuamini mtu ni lazima watoto tuwafatilie kwani watoto wetu wapo hatarini”, alisema Mkuu huyo.

Alieleza kuwa, mtuhumiwa hivi sasa yupo kizuizini chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi, na kuwataka wazazi kutoa ushirikiano katika kutoa ushahidi Mahakamani ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Mapema Katibu wa Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, alisema Ofisi ya Mufti imeamuwa kumfungia mwalimu huyo kwa tuhuma za udhalilishaji na kukosa sifa za kuwa mwalimu wa madrasa.

Alisema ofisi ya Mufti inasikitishwa na baadhi ya walimu kujihusisha na vitendo hivyo, na kusema kuwa lengo la kuwapeleka watoto madrasa ni kufunzwa elimu ya dini na sio kudhalilishwa.

Katika hatua nyengine, ofisi ya Mufti imeamuwa kuifungia madrasa hiyo kutokana na mazingira yasiyo rafiki na kubaini kuwa madrasa hiyo haikusajiliwa.

Aidha, Sheikh Khalid alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua kali dhidi ya mtuhumiwa mara tu baada ya kukamilika ushahidi wa tukio hilo.

Sambamba na hilo, alisema Ofisi ya Mufti Zanzibar inampango wa kuwapa mafunzo walimu wote wa madrasa Nchini, ili kuwawezesha walimu kujua maadili na misingi ya ualimu wa madrasa, kwa lengo la kuwanusuru watoto na vitendo vya udhalilishaji.

Pia, aliwaasa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao katika madrasa zenye mazingira salama, na zilizofuata utaratibu  ili kuwaweka watoto katika usalama.