Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Hussein Ali Mwinyi ameupongeza utayari
wa Jamhuri ya Ireland nchini Tanzania kwa kuahidi kuiunga mkono Serikali ya
Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi katika kuimarisha sekta zake
za maendeleo.
Rais Dk. Mwinyi
aliyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa
Jamhuri ya Ireland nchini Tanzania Bi Mary O’Neil aliyefika Ikulu kwa ajili ya
kujitambulisha.
Katika maelezo
yake Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi huyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya pande
mbili hizo, na kuupongeza utayari wa Jamhuri ya Ireland kuahidi kusaidia miradi
mbali mbali ya maendeleo.
Rais Dk. Mwinyi
alisema kuwa hatua za Jamhuri ya Ireland ya kuahidi kuwawezesha wanawake
kutasaidia kwa kiasi kikubwa hasa kwa upande wa wanawake wanaojishughulisha na shughuli
za kimaendeleo wakiwemo wakulima wa mwani ambao kwa upande wao wamekuwa na
changamoto ya kukosa soko la bidhaa yao hiyo.
Aidha, Rais Dk.
Mwinyi aliipongeza hatua ya nchi hiyo kutoa nafasi za masomo nchini humo na
kusisitiza haja ya kuendeleza na kuongezwa zaidi hatua hiyo ili Wazanzibari
walio wengi waweze kupata nafasi za masomo mbali mbali nchini humo.
Aliongeza kuwa
katika eneo la utalii, ambapo Balozi O’Neil aliahidi kwa nchi yake kwamba
atahakikisha anakuwa balozi wa kuitangaza na kuutangaza utalii wa Zanzibar
nchini mwake, alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kwani hivi
sasa wawekezaji katika sekta hiyo wamekuwa wakija Zanzibar na kuekeza kwa kasi
sambamba na kuongezeka kwa watalii kufuatia kupungua kwa janga la UVIKO 19
duniani.
Alieleza kuwa
suala zima la uhifadhi wa mazingira hasa katika bahari nalo limepewa kipaumbele
zaidi na Serikali ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuzuia
uharibifu wa mazingira huku akieleza kwamba licha ya kuwepo kwa mabadiliko ya
tabianchi na athari zake lakini bado hatua za makusudi zimekuwa zikichukuliwa
kuzibiti hali hiyo.
Kwa upande wa
Uchumi wa Buluu, Rais Dk. Miwnyi alimueleza Balozi huyo hatua na mikakati
iliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Nane huku akieleza kwamba Jamhuri ya Ireland
inasababu kadhaa za kuunga mkono hatua hizo hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo
imeweza kupiga hatua kupitia Dira hiyo.
Nae Balozi Bi
Mary O’Neil alimueleza Rais Dk. Mwinyi
azma ya Jamhuri ya Ireland ya kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza sekta
mbali mbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kuunga mkono hatua za kuwawezesha
wanawake, nafasi za masomo, mazingira ya upatikanaji wa haki kwa jamii, sekta
ya utalii, mabadiliko ya tabia nchi,
uchumi wa buluu na sekta nyenginezo.
Balozi O’Neil
alieleza jinsi Jamhuri ya Ireland ilivyokuwa na nafasi nzuri ya kuuunga mkono
Uchumi wa Buluu ambao ndio Dira ya Uchumi wa Serikali ya Awamu ya Nane chini ya
uongozi wa Rais Dk. Mwinyi hiyo ni kutokana na nchi hiyo kuwa na mazingira yanayofanana
na Zanzibar sambamba na kuitekeleza kwa vitendo Dira hiyo nchini humo.