Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)
limewaasa wananchi kutojihusisha na
utengenezaji, usambazaji, uuzaji au utumiaji wa mifuko na vifungashio vya
plastic visivyokidhi viwango kwa mujibu wa Sheria, kwani kufanya hivyo ni kosa
la Kisheria.
Tamko hili
limetolewa na Mkurugenzi wa Uzingatiaji
na Utekelezaji wa Sheria Bi. Redempta Samwel kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Baraza baada ya
kufanya ziara ya kushtukiza katika soko la Kisutu na Machinga Jijini Dar es salaam. Katika ziara
yake amebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wasiowaaminifu wanajihusisha na
uuzaji na usambazaji wa mifuko na vifungashio vya plastiki visivyokidhi vigezo.
Bi. Redempta Samweli amesema baada ya kufanya ukaguzi, viroba
zaidi ya hamsini vyenye vifungashio vya aina mbalimbali visivyokidhi viwango
vimekamatwa na vitaharibiwa na hatua zaidi za Kisheria zitachukuliwa dhidi ya
wanaohusika. Kufuatia changamoto hiyo, amewaambia watanzania kuwa ni marufuku
kutengeneza, kusambaza, kuuza au
kutumia mifuko na vifungashio
hivyo, kwani kufanya hivyo ni kukiuka Sheria.
“Tumefanya kaguzi na kukamata viroba zaidi ya hamsini vyenye
vifungashio vya aina mbalimbali vinavyotengenezwa hapa nchini visivyokidhi
viwango. Viroba hivi vitaharibiwa na hatua kali za Kisheria zitachuliwa dhidi
ya wanaohusika na zoezi hili ni endelevu. Kwa Sheria ya Mazingira na Kanuni ya
kudhibiti mifuko ya plastiki ya mwaka 2019 ni marufuku kutengeneza, kusambaza,
kuuza au kutumia vifungashio visivyokidhi viwango, kwani kufanya hivyo ni kukiuka Kanuni ya katazo la
mifuko ya plastiki. Kwa yeyote atakayebainikana na kosa hilo
tutamkamata na atachuliwa hatua za Kisheria.”
Sambamba na hilo Bi. Redempta Samwel, amewataka
watanzanzania kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni ili kuepuka migogoro na
Serikali na kuepuka gharama zisizokua za lazima.
“Niwaombe watanzania wote kwa ujumla, tutumie mifuko mbadala
na vifungashio vilivyoruhusiwa Kisheria na vyenye viwango ili kuepuka migogoro
na Serikali na kupunguza gharama zisizokuwa za lazima.”
Naye Bw. Hamadi Taimuru Kissiwa Meneja Kanda ya Mashariki
Kusini ameendelea kuwaasa wafanyabiashara na
wananchi kwa ujumla kutokuzalisha, kutokupokea, kusambaza na kutumia
mifuko na vifungashio visivyokuwa na viwango. Anasema watengenezaji wa
vifungashio visivyokua na viwango hawalipi kodi na vifungashio hivyo vinauzwa
kwa bei ya chini. Kufanya hivyo ni
kuikosesha Serikali mapato na kudhoofisha biashara ya wananchi wanaotengenza
mifuko na vifungashio kwa kuzingatia viwango.
“Tunawaasa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla
wasinunue,wasitumie wala wasisafirishe na
wasipokee kutoka kokote mifuko ambayo haikidhi viwango. Unaponunua bidhaa ambayo haijulikani
inatoka wapi na inamana hata kodi ya serikali halipwi, bidhaa nyingine hazina
viwango ina maana wale waliotekeleza viwango hawawezi kufanya biashara kwa
sababu wafanyabiashara wanaotengeza bidhaa ambazo hazikidhi viwango watauza kwa
bei ya chini hatimaye kuua soko la ushindani.”