MAONI YA WADAU JUU YA BAJETI YA SERIKALI MWAKA WA FEDHA 2022, 2023Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na wadau kutoka Mtandao wa Bajeti yenye Mlengo ya Jinsia ambao ni zaidi ya Asasi za Kiraia 100 na wanajamii kutoka mikoa mbalimbali wamekutana kujadili na kuchambua bajeti ya taifa ya mwaka wa fedha 2022/23 iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwingulu Lameck Nchemba, na baadae kutoa maoni yao yayotanguliwa na hali halisi ya uchumi wa Tanzania. 

 

Akizungumza wakati wa mjadala huo Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP,) Lilian Liundi amesema Bajeti hio ya mwaka wa Fedha 2022/23 ni bajeti ya pili katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa (FYDPIII) na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kutoa kipaumbele katika masuala ya usawa wa kijinsia.

 

Lilian amesema bajeti hio ina jitihada za kuboresha masuala ya kijinsia katika sekta mbalimbali, ambazo kwa kiwango kikubwa zinawagusa wanawake, vijana na makundi mengine yaliyoko pembezoni, hata hivyo, bado kuna maeneo yanayohitaji kufanyiwa kazi zaidi ili bajeti iwe chachu ya uchumi jumuishi kwa maendeleo ya watu.

 

Aidha wamesema wito kwa serikali kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa kulipa kodi na kuendelea kuwawajibisha maafisa wasio waadilifu wanaotumia kodi za wananchi kwa manufaa yao binafsi,na kubwa zaidi, kuhakikisha kuwa kodi zinazotolewa na wananchi zinaenda kuboresha maisha yao.

 

Ameongeza kusema kuwa ongezeko la bajeti ya Wizara ya Kilimo kilimo kutoka Bilioni 294 hadi Bilioni 954 inaonesha dhamira na nia ya dhati ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mh. Samia Suhulu Hassani kuleta mageuzi katika sekta ya Kilimo. Bajeti hii ya kilimo pia imelenga kuongeza ajira 3,000 kwa vijana, tunategemea kwa hali hii changamoto za ajira kwa vijana zitapata ufumbuzi kwa kiwango fulani.

 

‘’ Tunatoa wito kwaSerikali kuhakikisha kuwa vijana wote wa kike, wa kiume na wenye mahitaji maalumu wananufaika na ajira hizi zitokanazo na kilimo. Ikumbukwe kuwa kilimo kinaajiri takribani asilimia 58.1 ya watanzania, ambapo zaidi ya asilimia 80 ni wanawake.Hivyo, ni muhimu sana vijana wa kike nao wanufaike na bajeti hii ’’

 

‘’  Kwa upande wa Elimu, kufutwa kwa ada ya kidato cha tano na sita ni jambo la kupongeza kwa imani kuwa hatua hii itawapa fursa watoto wa kike kuepuka ndoa za utotoni hasa zile zinazotokana na kisingizio kuwa mzazi hana uwezo wa kumsomesha zaidi. Licha ya hatua hii nzuri, tutoa wito 

kwa Serikali kuzingatia uboreshwaji wa miundo mbinu na mazingira rafiki yatakayowawezesha watoto wa kike na wale wenye ulemavu kusoma bila changamoto  ’’

Mkutano wa mjadala huo umeandaliwa  na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP,) na kuwashirikisha wananchi, wanajamii, wachambuzi, wanasiasa na wanachama wa mtandao huo na kusikiliza kwa pamoja uwasilishwaji wa bajeti ya Taifa na kutafakari na kujadili kwa mlengo wa kijinsia kwa namna ambavyo bajeti kuu imeakisi kupitia sauti za wanajamii.