SERIKALI YALAANI TUKIO LA KUVAMIWA NA KUPIGWA KWA MWANASIASA BARAKA SHAMTE

 


SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar inalaani vikali tukio la kupigwa kwa mwanasiasa mkongwe Bwana Baraka Mohamed Shamte lililotokea hapo jana.

 

Katika tukio hilo inasemekana kwamba mwanasiasa huyo amejeruhiwa katika baadhi ya sehemu zake za mwili tukio ambalo lilipelekea kupata maaumivu makali na hatimae kukimbizwa hospitali.

 

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatoa pole kwa mwanasiasa huyo mkongwe na kuahidi kwamba inalichunguza tukio hilo na kuhakikisha kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama vinawatia mbaroni wahusika.

 

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inapinga vitendo vya watu kujichukulia sheria mikoni na kuwataka watu kuwa watulivu wakati vyombo husika vinalifanyia kazi suala hilo.