UTENZI MAALU WA SENSA YA WATU NA MAKAAZI TANZANIA

   1. Bismilahi rabuka

Wahadau lasharika
Kuondoa na kueka
Nikazi yake jalia

2. Muumba na muumbua
Katika hii dunia
Atakacho taka hua
Hakuna wa kuzuiya

3. Kwaio tujitahidi
Tusimuuzi wadudi
Tuvute sana nyiradi
Mungu kumnyenyekea

4. Ili mwisho mwema sote
Hapa tulipo tupate
Shetani asituvute
Tukaenda kuunguwa

5.Nisende sana usoni
Kusoma hawachosheni
Wacha kwenye madhumuni
Ya tenzi ningeingiya

6.Lengo na langu dhumuni
Ya tenzi hii jamani
Kutunga niwambieni
Ni sensa mngetambuwa

7.Agosti  mbili tatu
Ndio ile siku yetu
Ya sensa enyi watu
Tukae tukitambua

8.Akipenda ya razaku
Tukafika iyo siku
basi tuwe nashauku
Sensa kutufikiya

9.Siku iyo maalumu
Yakupata takuimu
Ya watu na yasehemu
Ya makazi tanzania

10.Siku hio hala hala
Tusijekwenda pahala
Ndani mwako wewe lala
Ungoje kuhesabiwa

11.Msijekwenda kondeni
Kwenda kutafuta kuni
Au maji visimani
Nyumba mkazikomea

12.Siku iyo vikobani
Kina mama vikundini
Msende pumzikeni
Mngoje kuhesabiwa

13.Na nyinyi akina baba
Msije kutoka raba
Kabla kupita esaba
Ya sensa ninawambia

14.Ata sheli usiende
Umngojee afande
Karani mwenye kipande
Hesabuni kukutiya

15.Awaulize maswali
Machache lile na hili
Ni kama dakika mbili
Atakazo zitumia

16.Walemavu majumbani
Tusiwafiche jamani
Nawao wawe kundini
Tuhesabiwe pamoya

17.Nawao tasaidiwa 
Mambo yao kupangiwa
Serekali kiwajuwa
Huduma tawafikia

18.Mila potofu jamani
Tuziekeni pembeni
Sote natushirikini
Tuijenge tanzania

19.Tusisingizie dini
Tukajiweka pembeni
Sio dhambi asilani
Sensa si jambo baya

20.Jamii ya wafugaji
Hasa katika vijiji
Sensa yawahitaji
Msije mkakimbia

21.Hili jambo sio geni
La sensa tutambueni
Tokea mwaka sitini
Ndiko liliko anziya

22.Sensa faida yake 
Kwa nchi iyeleweke
Ni kujua watu wake
Na makazi wanokaa

23.Mipango ya serekali
Nayo takua jamili
Huduma zilokamili
Wananchi tafikiya

24.Ili ikija misada 
Pasikuepo na shida
Kwenye kugawa faida
Ya sensa nawaambia

25.Mtakapo ihalifu
Sensa nawaarifu
Kitacho jiri sarafu
Yetu tunayo tumiya

26.Tutaiangusha chini
Uzidi umasikini
Nanjaa itukafini
Kaburini kututia

27.Uchumi utadorora
Badala kua imara
 hii yote ni hasara
Yakuto kuhesabiwa

28.Pia masipitalini
Madawa vidirishani
Msije kosa husseni
Paka mkamrushiya

29..Wakati nyinyi wenyewe
Ndo mlo tenda yawe
Haya mambo sio yeye
Alo tusababishia

30.Muda ushatarazaki
Nataka iwacha chaki
Ila sitotenda haki
Kama sitowawekea

31.Jina langu mtungaji
Na namba mkihitaji
Ruhusa sitowahoji
Nani amekupatia

32.Jina aliy samsoni
Kinda wa kidarajani
Ndie nilo shika peni
Utenzi kujitungiya

33.Namba zangu zero sita
Tano tano ninapita
Mbili mbili nne sita
Nne nne malizia

34.Izo ndio namba zangu
Za simu tangu na tangu
Nahapa ndo mwisho wangu
Wa tenzi ninaishia.

UTENZI WA SENSA.
MTUNZI ALI SAMSON (MTUNZI KINDA 
MAKAZI KWAALAMSHA KIDARAJANI
ZANZIBAR, 0655224644.