ZIC YAHITIMISHA MAADHIMISHO YA MIAKA 53 KWA KUZINDUA “ZIC APP

 


Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) limehitimisha maadhimisho ya miaka 53 tangu kuanzishwa kwake kwa kuzindua program ya online (Online App) ijulikanayo kama ZIC App ikilenga kusogeza huduma zake karibu zaidi na wateja.


Uzinduzi wa Programu hiyo ulifanyika mwishoni mwa wiki visiwani humo wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Shirika hilo kwa ajili ya wadau wake mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo, hafla ambayo ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa serikali, wateja na wageni waalikwa kutoka mashirika na taasisi mbalimbali.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Ali Suleiman  aliemuwakilisha Waziri wa Wizara hiyo Bi Saada Mkuya alisema mafanikio hayo yanaashiria kwamba hilo shirika hilo lipo imara kiutendaji hatua ambayo inaithibitishia serikali kuwa umefika muda muafaka kuweza kulipatia uhuru wa kujiendesha kiushindani ili liweze kutengeneza faida zaidi.

“Maendeleo haya makubwa tunayoyashuhudia yakiwemo ya kiteknolojia yanatuongezea imani kwamba sasa umefika wakati tuwape uhuru zaidi ili muweze kujiendesha kwa ushindani na kusimamia mambo yenu bila kuingiliwa wala kuhodhiwa sana na serikali,’’ alisema.

Hata hivyo alibainisha kuwa changamoto kubwa iliyo mbele ya shirika hilo ni kuhakikisha kuwa linasogeza zaidi huduma zake hadi vijinini ambapo kuna idadi kunwa ya wananchi hususani wakulima, wavuvi na wafanyabiashara wadogo ambao hawajafikiwa na huduma hiyo.

“Ni dhamira ya serikali kuona kwamba huduma za kibima zinaelekezwa pia kwenye maeneo ya pembezoni ambako kuna wananchi wengi ambao nao wanaohitaji kupatiwa huduma za bima. Wananchi wengi wanapoteza mitaji na mazao yao katika maeneo mbalimbali kutokana na majanga mbalimbali hivyo ni matarajio ya Serikali kuwa huduma zenu zitawagusa zaidi hao pia.’’ Alisema.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa ZIC Bw Arafat Haji alisema ukuaji wa shirika hilo unaoshuhudiwa kwasasa ni matokeo ya ushirikiano baina yake na wadau wake wakiwemo wateja na washirika kibiashara likiwemo Shirika la Posta Tanzania ambao kupitia ushirikiano wao wameweza kujitanua nchi nzima.

“Pamoja na yote hayo ni kwa muda mrefu sasa ZIC tumekuwa tukijikita zaidi kwenye uwekezaji wa mifumo ya kidigitali itakayotuwezesha kuwafikia wateja wengi zaidi, kwa urahisi zaidi, mahali popote walipo na hivyo kuwaondolea wateja wetu ulazima wa kutembelea matawi yetu pindi wanapohitaji huduma zetu…ujio wa ZIC App ndio kilele cha mafanikio hayo,’’ alisema.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Kamishna Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Bi Khadija Said pamoja na kulipongeza shirika hilo kwa mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka 53, alitoa wito kwa makampuni ya bima nchini kuendelea kubuni zaidi huduma mbalimbali za kibima ili kuongeza wigo wa huduma za kibima sambambana na njia (distribution channels) za kuwafikia wateja wao.