KILIO CHA WENYE ULEMAVU SEKTA YA AFYA KINAHITAJI KUNYAMAZISHWA .

 




Licha ya serikali kufanya jitihada za kuona wananchi wake wanapata huduma bora za afya kwa kujenga vituo vya afya maeneo ya karibu na makaazi ya wananchi, ununuzi wa dawa pamoja na ununuzi wa vifaa tiba, lakini bado inaonekana kundi la watu wenye ulemavu limesahaulika.

 

Wakizungumza na mwandishi wa makala haya kwa masikitiko watu wenye ulemavu, wamesema pamoja na kilio wanachokitoa mara kwa mara kwa viongozi na serikali kwa ujumla katika upatikanaji wa huduma bora za afya bado kilio hicho hakijapata mnyamazishaji.

 

Miongoni mwa huduma ambazo watu wenye ulemavu wamekuwa wakizililia ni ukosefu wa wakalimani wa lugha ya alama, dawa za ngozi kwa wenye ualibino, miundombinu kutokuwa rafiki kwenye Hospitali bado utekelezaji wake unasusua hali hadi leo.

 

“Baadhi ya wakati ninapokuwa na maradhi huona ni bora kukaa nyumbani na maradhi yangu, kuliko kwenda Hospitali, kwani hata nikienda hospitali ni kujiongezea maradhi mengine tu” alisema Abdul-azizi Khamis miaka (27) mkaazi wa Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja ambaye ni mlemavu wa usikivu (Kiziwi).

 

Abdul-azizi amesema kwamba hatua hiyo huja hasa baada ya kukosa mtu wa kwenda naye Hospitali ambaye ana taaluma ya lugha ya alama ambaye huwa ni mkalimani wake anapokutana na Daktari.

 

“Kwa kweli tunasumbuka sana tukienda Hospitali bila ya kuwa na wakalimani wa lugha ya alama, kutokana na Madaktari wengi kutokuwa na uelewa wa lugha za alama hivyo huwa hatufahamiani au wengine hutupuuza kabisa”alisema.

 

Hata hivyo Abdul-azizi amesema baadhi ya wakati huwa na hofu kwamba, hata akienda Hospitali anaweza kupata tiba au dawa ambazo hazihusiani na maradhi yanayomsumbua, hiyo ni kutokana na Madaktar mara nyingi huonekana kubahatisha tu katika utoaji wa tiba kwa wagonjwa wenye Uziwi.

 

“Katika hilo mimi nimeshawahi kukosa tiba kutokana na ukosefu wa kusikia, nilikuwa nje ya chumba cha Daktari nikisubiri zamu yangu, kumbe Daktari alikuwa anaita tu jina langu mimi wala sisikii, hivyo akaona kwamba anayeitwa itakuwa ameshaondoka kumbe nipo”alisema.

 

Amesema kitendo hicho kwa kweli kilimuathiri sana na ndicho kilichomfanya kukosa hamu ya kwenda Hospitali bila ya kuwa na mkalimani, akishauri kwamba ili Viziwi waweze kupata huduma bora za afya kuandaliwe wakalimani katika vituo vyote vya Afya pamoja na Madaktar kupewa elimu ya Ukalimani.

 

Mzee Khatib Kheri mwenye mtoto mwenye ulemavu wa akili ambaye anakabiliwa na maradhi ya kiafyua, amesema suala la upatikanaji wa dawa katika hospitali bado ni kikwazo kwa kundi hilo, hali ambayo huwapa wakati mgumu katika maisha yao.

 

Alitolea mfano wa mtoto wake kwamba hulazimika kutoa shilling 1400, ni kiwango kidogo ila kwa upande wa ni kikubwa hasa kwa kuwa dawa hizo huhitajika kila siku.

 

Naye Bi Mwaisha Shaaban ambaye ni mama wa Mtoto mwenye ulemamvu wa viungo amesema suala la miundombinu kwa wenye ulemavu wa viungo bado ni kikwazo katika upatikanaji wa huduma bora.

 

Alisema hospitali nyingi hazina visaidizi kwa watu wenye ulemavu hasa kwa Hospitali za ghorofa, hivyo wanapofika watu wenye ulemavu wa viungo huwa ni vigumu katika kupata tiba.

 

“Inatokea tiba zipo ghorofa ya juu, hivyo mzazi au mlezi anayekwenda na mgonjwa hutumia nguvu zaidi ya kumbeba mgonjwa wake, kitendo ambacho si kizuri hata kidogo“alisema Bi Mwanaisha.

 

Alisema kwa hali kama hiyo baadhi ya wakati huyo msaidizi wa mgonjwa hupata maradhi yeye anaporudi nyumbani kutokana na nguvu anazotumia kwa ajili ya kumfanikishia mgonjwa wake matibabu.

 

“Mbali hilo lakini pia umbali wa vituo vya daladala na vituo vya afya nalo ni changamoto kubwa, maana mtu ukishashuka hulazimika kutumia nguvu nyengine kama huwa Baiskeli ya kumsaidia,itakulazimu kumbeba au kumlazimisha kwenda kidogo kidogo”alisema.

  

Wadau watema cheche

 

Mkurugenzi Mtendaji Jumuiya ya Wakalimani wa lugha ya alama Zanzibar (Juwalaza), Kheri Mohamed Simai amesema kwa ujumla huduma za afya kwa wenye ulemavu hasa Viziwi ni kikwazo kikubwa ambacho kinahitaji utatuzi wa haraka.

 

Amesema kuna matukio mbali mbali wamepokea kutoka kwa agonjwa wenye Uziwi, ambayo wamekumbana nayo Hospitali, kitendo ambacho kikipuuzwa kinaweza kuongeza ugonjwa zaidi kwa Viziwi na wenye ulemavu kwa ujumla.

 

“kuna tukio tulipokea kwamba kuna mgonjwa kiziwi ameenda Hospitali kimatibabu, Dokta alimpa dawa kwa kubahatisha tu kutokana na kutofahamiana lugha, lakusikitisha yule mgonjwa alimeza dawa zile na kupata madhara makubwa”alisema.

 

Mbali ya hilo alisema pia kuna tukio la kiziwi ambaye ameenda Hopsital kujifungua (kuzaa), akiwa kitandani akijihisi muda wake wa kujifungua umefika kila akimwita Dokta kwa ishara Dokta hamsikii wala hamfahamu kutokana na Uziwi wake, hatimae yule mgonjwa alijifungua na kupata madhara kiafya.

 

“Mbali ya matukio hayo kuna matukio mengi tu ambayo wanakumbana nayo wagonjwa ambao ni Viziwi, kitendo ambacho baadhi yao huona ni bora kukaa nyumbani wanapotapa maradhi kuliko kwenda hospital, jambo ambalo halikubaliki kiafya pamoja na Haki za Binadamu”alisema.

 

Kheri ambaye ni Muuguzi wa Afya kitaalam amesema awali alikuwa na shauku ya kusomea ualimu ili kutumia taaluma yake ya Ukalimani kusaidia wanafunzi Viziwi, lakini baada ya kuona kundi kubwa la Viziwi wanasumbuka kiafya, aliona amsomee masuala ya Uuguzi wa Afya.

 

“Kwa sasa nipo Hospital ya Mnazi mmoja nikiwa pia ni Mkalimani wa Lugha za alama kwa magonjwa Viziwi, lakini ukubwa wa Hospital na wingi wa wagonjwa siwezi kuwafikia wagonjwa wote Viziwi wanaofika Hospitalini hapo kimatibabu’ alisema.

 

Alisema kupitia Jumuiya yao wameanza harakati za kuona kundi hilo linapatiwa tiba bora kwa kutatuliwa changamoto zao, miongoni mwa juhudi hizo ni kuzungumza na Serikali juu ya kuwasomesha baadhi ya watendaji na wafanyakazi wao Lugha za alama.

 

Alisema pia wameshawishi kila Hospital awepo Mkalimani ijapokuwa kati ya Madaktar au waunguzi, lengo ni kusaidia kundi la wagonjwa Viziwi watakaokwenda kwa ajili ya matibabu, lakini pia wameshauri kuwepo miundombinu imara na rafiki kwa watu wenye ulemavu katika Hospital.

 

Kheri alisema pia wameanza mazungumzo na Wizara ya afya ili kutolewa kwa vitambulisho maalum kwa watu wenye ulemavu, ili kuwa rahisi wanapofika Hospital kupatiwa tiba bila ya usumbufu.

 

Naye Katibu Jumuiya ya Wasioona Zanzibar (Zanab) Adil Mohamed Ali alisema licha ya kupeleka maombi na kukubali juu ya kuwekwa vibao katika Hospital juu ya ruhusa kwa dala dala kushasha abiria mwenye ulemavu, lakini bado inaonekana utekelezaji wake haujawa mzuri.

 

Alisema ni vyema jambo hilo likachukuliwa kwa umakini mkubwa ili kuona kundi la watu wenye ulemavu linapata huduma bora za kiafya na nyengine, akisisitiza haja ya Serikali kuvalia njuga suala hilo.

 

Adil ameshauri wa Serikali kutenga bajeti maalum katika fungu la afya kwa watu wenye ulemavu ili wale wanaosumbuliwa na maadhi sugu hasa Albino waweze kupata tiba iliyo bora na sahihi.

 

Akizungumzia miundombinu alisema bado si rafiki kwani baadhi ya maeneo ni vigumu kufikika kama hakuna miundombinu bora katika Hospital hasa kwa zile Hospital za Ghorofa lakini zina uhaba wa Lifity.

 

Kwa upande wa Mshauri elekezi ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar (Juwauza), Suleiman Baitan alisema umefika wakati sasa kwa serikali na wadau mbali mbali kuimarisha miundombinu mbali mbali ili kuwa rahisi kufikika kwa watu wenye ulemavu.

 

Alisema ni wazi kwamba miundombinu isipoimarisha na kuboreshwa inaweza kuleta madhara au kuongeza idadi ya watu wenye ulemavu, jambo ambalo kwa sasa halihitaji hata kidogo kuona idadi inaongezeka kwa mambio ambayo yanweza kutaulika.

 

 Afisa maendeleo ya jamii kutoka Madrasa Early Child Hood , Mohamed Othman Dau amesema licha ya uwepo changamoto mbali mbali kwa watu wenye ulemavu, lakini bado wazazi na jamii kwa ujuml inapaswa kufahamu kwamba kundi pia linahitaji kupatiwa haki kama yalivyo makundi mengine.

 

“Ulemavu sio jambo la kumfanya mtu akose fursa zake za msingi ikiwamo kiafya, kijamii, kiuchumi na hata kisiasa au aonekane kuwa ni mtu tofauti hapana tukifanya hivyo tutakuwa hatuwatendei haki” alisema .

 

Serikali nayo yaeleza

 

Licha ya uwepo a changamoto mbali mbali katika upatikanaji wa huduma za afya kwa watu wenye ulemavu, serikali nayo imesema kuna mipango inafanyika ili kuona kundi hilo haliachwi nyuma kama ilivyo sasa.

 

Naibu Katibu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Abeda Abdalla Rashid alikiri kuwepo kwa changamoto za kiafya kwa watu wenye ulemavu, akihidi kwamba Serikali imejipanga vyema katika kukabiliana na hali hiyo.

 

Alisema katika kulifanikisha hilo kupitia ujenzi wa Hospital 10 zaitakazojengwa kupitia fedha za mkopo za IMF, Serikali imedhamiria Hospital hizo kuwa na vifaa na miundombinu kamili ili watu wenye ulemavu waweze kuzitumia na kupata tiba bila ya usumbufu.

 

Kuhusu suala la Wakalimani wa lugha za alama katika Hospital alikiri kwamba hadi sasa kuna uhaba mkubwa, akitolea mfano kwa Hospital za Unguja kuna wakalimani wawili tu ambao hufanya kazi muda mwingi, akibainisha kwamba serikali imeliona hilo na litafanyiwa kazi.

 

Kuhusu suala la dawa kwa wenye Ualibino awataka Albino kufika katika vituo vya afya mara kwa mara, akibainisha kwamba baadhi ya wakati dawa huwemo lakini wao ndio huwa shida kufika vituoni kwa ajili ya kuchukua dawa za kulinda ngozi zao.

 

Abeda ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, anasema ili changamoto za watu wenye ulemavu ziweze kutaulika vyema, umefika wakati wa kuwepo Baraza la ushauri ambalo litajumuisha taasisi mbali mbali ambazo zinahusika na watu wenye ulemavu.

 

Kwa upande wa Mkurugenzi Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Ussi Khamis Debe amesema katika kuhakikisha suala la watu wenye ulemavu linafahamika vyema, wameanza na usajili ili kuwatambua watu wote wenye ulemavu visiwani hapa.

 

Alisema hadi kufiki sasa zaidi ya watu 8,000, wameshasajiliwa na kutambulika rasm na Idara yake, pamoja na aina za ulemavu walionao, ambapo kazi ya usajili inaendelea kwa maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.

 

Alisema ni wazi kwamba mfumo wa utambulisho wa watu wenye ulemavu utsaidia katika upatikanaji wa huduma mbali mbali za kiafya, kielimu na nyenginezo, hivyo ameomba wenye watu wenye ulemavu au wazazi na walezi kujitokeza pake wanapohitajika taarifa zao.

 

Hata hivyo juhudi zinahitajika kwa Serikali na wadu mbali mbali kuhakikisha haki za watu wenye ulemavu hasa katika afya zinatekelezwa kama mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu unavyoelezwa, kwamba

 

Nchi zilizoridhia mkataba huo zina wajibu kutambua kwamba watu wenye ulemavu wana haki ya kupata huduma za afya bila ya ubaguzi.


Makala kutoka kwa Haji Mtumwa, Zanzibar.