WANAKIJIJI BINGUNI WATAKIWA KUANZISHA ULINZI SHIRIKISHIWananchi wa Kijiji cha Binguni wameshauriwa  kuanzisha kikundi cha ulinzi shirikishi ili kujikinga na vitendo vya kihalifu vinavyoweza kujitokeza katika jamii.

Akizungumza na wakaazi wa Shehia ya Binguni (TRO) Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Salama Juma Salum amesema ushirikishwaji wa jamii katika ulinzi shirikishi utasaidia kupunguza vitendo vya kihalifu ambavyo vinashamiri siku hadi siku .

Amesema Serikali iko tayari katika kupambana na vitendo vya kihalifu ikiwemo wizi na utumiaji wa dawa za kulevya jambo ambalo linaathiri familia na jamii kwa ujumla.

Aidha amefahamisha kuwa katika kupambana na vitendo hivyo lazima jamii ishirikiane na Serikali katika kutoa taarifa pindi ikitokea ishara ya vitendo hivyo ili kudhibiti hali hiyo isiendelee kuwepo.

Akifafanua makosa ambayo hayatakiwi kupangiwa sheria ndogondogo Msaidizi huyo amezitaja ni ubakaji na dawa za kulevya  lakini kuna baadhi ya watu hawatoi taarifa hizo jambo ambalo linarejesha nyuma jitihada za Serikali.

 Hata  hivyo amewashauri wakaazi hao  kushirikiana  kwa pamoja katika ulinzi na kuanzisha sheria ndogondogo ambazo zitawasaidia kutatua changamoto zinazowakabili  sambamba na kuanzisha mazizi ya ng’ombe salama ili kujikinga na vitendo hivyo.

Nae Sheha wa Shehia hiyo Ali Yussuf Mussa  amesema uingiaji wa wageni kiholela unapelekea kujitokeza vitendo vya uhalifu na kuwataka vijana kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha katika kushiriki katika ulinzi shirikishi ili kukabiliana na vitendo hivyo.

Nao wakaazi wa shehia hiyo wameomba kupatiwa ulinzi wa doria hasa wakati wa mchana ambapo  wanyama wao wanaibiwa  kwa wingi.