Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed amewataka Madaktari wa Hospitali mbalimbali hapa nchini kuwa waadilifu katika kutekeleza wa kazi zao za kuwahudumia wananchi kwani kufanya hivyo ni kuimarisha dhana nzima ya Mapinduzi ya mwaka 1964
Ameyasema hayo huko Makunduchi Mkoa wa kusini Unguja wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi katika Jengo la Maradhi ya Dharura na Maabara katika Hospitali ya Makunduchi Koba.
Amesema kuwa dhana nzima ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo ya huduma bora ya matibabu ili kuepukana na adui maradhi ambayo yanawasumbuwa binadamu na kuwa dhaifu.
Amesema kuwa katika Maadhimisho hayo ya miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar mambo mengi yamefanyika yakiwa na dhamira ya dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi wake pamoja na kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Aidha aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya pamoja na washirika wa kimaendeleo kwa juhudi zao za kuhakikisha kwamba wananchi wanapata mahitaji yao katika sekta ya Afya.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Fatma Mrisho amesema Wizara ya afya itaendelea kuwapatia huduma bora wananchi pamoja na mafunzo kwa wataalamu wake.
Aidha alisema watalamu hao watawapatia mafunzo pamoja na kuweka vifaa bora, madawa na huduma nyengine muhimu.
Hata hivyo alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Helth Imrovement Project (HIPZ) wanajenga jengo la kisasa kwa huduma ya Maabara
Nae Mkurugenzi wa Shirika la Health Improvement Project Zanzibar (HIPZ) Simon Kuhoert amesema zaidi ya shilling Milioni mia 570 zimetumika kwa ujenzi wa Maabara hiyo.
Alisema Shirika lake litaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutoa misaada mbali mbali ambayo ni mahitaji ya msingi kwa Wagonjwa.
Nae Daktari dhamana wa Hospitali ya Makunduchi Mohamed Mtumwa Mnyimbi ameahidi kuziunga mkono juhudi za Serikali kwa kuhakikisha wanalienzi jengo hilo na kufuata maadili ya kazi zao.
Aidha alitaja baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo ni pamoja na uchahakavu wa nyumba za Madaktari , upungufu wa wafanyakazi wa Hospitali uzio wa Hospitali hiyo pamoja na ubovu wa barabara .